WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano ipo macho, haijalala na haijashindwa kuongoza nchi bali imejipanga kuliongoza Taifa kwa mafanikio makubwa.
"Serikali haijashindwa kuongoza nchi. Nataka niwahakikishie waheshimiwa Wabunge na wananchi wote kwamba tutaongoza nchi hii kwa mafanikio makubwa na kazi hiyo imeanza kwa marekebisho makubwa kwa maeneo ambayo tunadhani yatafanya Taifa hili liweze kupata mafanikio makubwa,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi, Septemba 8, 2016) Bungeni mjini Dodoma wakati akijibu swali lililoulizwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani Bungeni na Mbunge wa Hai, Bw. Freeman Mbowe, ambaye alitaka kufahamu Serikali ina mkakati gani wa kunusuru mdororo wa uchumi uliopo nchini.
Bw. Mbowe alidai kwamba hali ya uchumi imeshuka na kwa mujibu wa taarifa za Benki Kuu ya Tanzania (BOT) uagizaji wa bidhaa kutoka nje umepungua, uuzaji wa bidhaa nje ya nchi na sekta ya ujenzi imesimama hali inayoashiria kudorora kwa uchumi.
Kuhusu suala la kupungua kwa mizigo katika bandari na vituo vya forodha, Waziri Mkuu amesema usafirishaji wa mizigo kwa njia ya bahari umeshuka duniani kote kwa sababu ya kushuka kwa hali ya uchumi kutokana na kuporomoka kwa bei ya mafuta na gesi.
Hata hivyo Waziri Mkuu amesema tayari wafanyabiashara wa Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC) wameihakikishia Serikali kwamba mizigo yao yote itakuwa inapitia Bandari ya Dar es Salaam hasa kwa mkakati wa pamoja wa ujenzi wa reli ya standard gauge inayoanzia Dar es Salaam-Tabora - Isaka.
Wakati huo huo Waziri Mkuu amesema Serikali itahakikisha inaendelea kuimarisha amani na ulinzi kwenye maeneo yote nchini na kwamba vyombo vya dola viko macho. “Watu wote wanaojihusisha na vitendo vya uhalifu yakiwemo mauaji watakamatwa popote walipo na kuchukuliwa hatua za kisheria,; amesema.
Amesema hatua hiyo inatokana na matukio ya mauaji yaliyotokea hivi karibuni ambapo raia wasiokuwa na hatia na askari waliuawa katika maeneo ya Vikindu mkoani Pwani, Tanga na Mwanza. Waziri Mkuu ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Korogwe Vijijini, Bw. Stephen Ngonyani
Katika swali lake, Bw. Ngonyani alitaka kujua ya Serikali kuhusu kukomesha mauaji hayo, yanayotokea kwa watu wasio na hatia pamoja na askari, ambapo Waziri Mkuu, alitumia nafasi hiyo kutoa pole kwa wananchi na familia, ambazo ndugu zao walipoteza maisha katika mauaji hayo.
Pia ametoa wito kwa Watanzania wote kuhakikisha wanawafichua watu ambao wanawatilia shaka na kutoa taarifa kwa vyombo vya dola ili waweze kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua