TAMKO LA WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KUHUSU WATOTO WALIOMALIZA ELIMU YA MSINGI 2016

TAMKO LA MHESHIMIWA UMMY MWALIMU (MB) WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO KUHUSU WATOTO WALIOMALIZA ELIMU YA MSINGI LILILOTOLEWA TAREHE 09/09/2016

Ndugu Wanahabari, Nitumie fursa hii kupitia kwenu kuongea na watoto wa Tanzania, wazazi / walezi na jamii kwa ujumla katika kipindi hiki muhimu ambacho watoto wetu wamemaliza Elimu ya Msingi.  Kwa niaba yangu na kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania napenda kuchukua nafasi hii kuwapongeza watoto wote waliomaliza mtihani wa Taifa wa kuhitimu Elimu ya Msingi mwaka huu, Hongereni sana!. Ni jambo la ufahari kwetu sisi wote kama wazazi/ walezi na Taifa kwa ujumla kwani hii ni fursa adhimu kwa ustawi na maendeleo ya mtoto na ni moja ya njia ya kutimizwa kwa haki ya msingi ya mtoto ya kuendelezwa ambayo inamjengea mtoto msingi imara wa maisha yake ya baadae. Pongezi zangu nyingi kwa watoto wote wa kike na wa kiume walioweza kufikia hatua hii muhimu kwa maendeleo na ustawi wao.

Ndugu Wanahabari, Takwimu zinaonyesha kuwa, wanafunzi 795,761 (wavulana 372,883 sawa na asilimia 46.86 na wasichana 422,878 sawa na asilimia 53.14) wamesajiliwa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka huu. Hivyo ningependa kutumia fursa hii kuwaasa watoto waliomaliza darasa la saba kutojihusisha na tabia au vitendo vyovyote vinavyo hatarisha afya, usalama na maendeleo yao, kama vile kujihusisha kwenye masuala ya ngono, matumizi ya madawa ya kulevya na vileo katika kipindi hiki cha kusubiri matokeo ya mitihani yao.

 Watoto wetu wa Kike na Kiume wajitambue, na wajue kuwa wao ni hazina ya pekee katika maendeleo ya nchi yetu. Kipindi hiki wakitumie vizuri kwa kuwa waadilifu, waaminifu, wenye bidii na kuzingatia kanuni za nidhamu na tabia njema huku wakijiandaa kwa ajili ya kuendelea na elimu ya Sekondari. Tukumbuke kuwa Serikali imekusudia kumpa kila mtoto nafasi ya kupata elimu ya Sekondari. Msingi tayari umeshawekwa na Rais wa Awamu ya tano, Mheshimiwa John Pombe Magufuli wa kutoa Elimu ya Sekondari bure. Hivyo tusingefurahi mmojawapo kati ya watoto hawa waliomaliza elimu ya msingi jana akaikosa nafasi hii kwa sababu zinazoweza kuzuilika. Nawaasa watoto wote kutumia kipindi hiki kwa kukataa kurubuniwa, kushawishiwa na kujiingiza katika mambo yenye kuhatarisha afya, usalama na maendeleo yao.

Ninawataka Wazazi wenzangu, Walezi na jamii kwa ujumla:-
Kutowaozesha watoto wote wa kike waliohitimu darasa la saba mwaka huu wakati wa kipindi hiki cha kusubiria matokeo yao, iwe ni kwa sababu yoyote ile au kwa lengo la kujipatia mali kwa njia ya mahari. Kila Mzazi/Mlezi anapaswa kutambua umuhimu wa mtoto wake kuendelea kielimu, na kukua kimwili na kiakili kabla ya kuingia katika ndoa. Ieleweke kuwa Elimu ya watoto wa kike ni moja ya njia bora za kupunguza umaskini katika mataifa yanayostawi. Kila mwaka wa elimu kwa mwanamke utaongeza mapato yake ya baadae kwa asilimia 15, ikilinganishwa na asilimia 11 kwa wanaume. Aidha, Kila mwaka wa mtoto wa kike kuwa shule humuepusha na maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) mara 7.

Pia, uzoefu unaonyesha kuwa, kila mwaka wa kuelimika humsaidia msichana kufanya maamuzi bora yake na ya familia yake. Benki ya Dunia ilibainisha ya kwamba kila mwaka wa elimu huzuia vifo 2 vya uzazi katika wanawake 1000 kila mwaka!. Kwa hiyo kumpa mtoto wa kike fursa ya elimu inamsaidia sio yeye tu kukua kiakili na kimwili lakini pia inamnusuru na ndoa na mimba za utotoni na kuchangia maendeleo yake, ya familia yake na jamii kwa ujumla. Ni vyema jamii hasa wazazi na walezi wafahamu kuwa ndoa kwa wasichana sio njia muafaka ya kutatua changamoto za kifedha za wazazi/walezi. Bali elimu ndio njia bora ya kutatua changamoto hizo.

Kuwalinda watoto wote wa kike na wa kiume waliohitimu darasa la saba mwaka huu dhidi ya vitendo vyote vya Ukatili, hasa kwa watoto wa kike kupewa mimba au kuwahusisha katika mahusiano ya kimapenzi. Kwa mujibu wa Sheria ya makosa ya kujamiiana ya mwaka 1998 ambayo imefanyiwa marekebisho na kuhuishwa kwenye Makosa ya Jinai (Penal Code Cap 16)  inaelekeza kuwa ni kosa la jinai  kwa mtu yoyote kumlaghai mtoto wa chini ya miaka  18 kwa kumpa mimba au kufanya nae mapenzi.

 Kifungu cha 130 (e) cha Sheria hii kinaeleza wazi kuwa “Ni kosa kwa mtu wa jinsia ya kiume kumbaka msichana au mwanamke; kwa ridhaa au bila ya ridhaa akiwa chini ya umri wa miaka kumi na nane. Mtu yeyote atakayetenda kosa la kubaka atawajibika kwa adhabu ya kifungo cha maisha au kifungo kisichopungua miaka thelathini. Aidha, Sheria ya Mtoto Namba 21 ya mwaka 2009 Kifungu cha 83 kinaelekeza kuwa ni kosa kumuhusisha mtoto katika kazi, biashara au mahusiano yoyote yenye mlengo wa kingono iwe ni kwa malipo au bila malipo.

Mkono wa Serikali ni mrefu. Tutahakikisha tunawakamata na kuwafikisha Mahakamani wale wote watakao kwenda kinyume na sheria hizi.

Aidha, natoa Rai kwa wananchi wote kuendelea kutoa taarifa kwa mamlaka husika za Serikali za Mtaa, Kijiji, Kata, Wilaya na hata katika Madawati ya Jinsia na Watoto yaliyopo Polisi, pale watakapobaini mzazi au mlezi au taasisi anaenda kinyume na jitihada za serikali za kumuendeleza mtoto kielimu hasa katika kudhibiti ndoa za watoto waliomaliza Elimu ya Msingi hususan katika kipindi hiki cha kusubiri matokeo yao.

Vunja ukimya toa taarifa kwa maendeleo ya watoto wetu.
Nawatakia kila la kheri watoto wote wa Tanzania katika kipindi hiki cha kusubiri matokeo yao ya mtihani wa Elimu ya msingi.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu wabariki watoto wa Tanzania.

Imetolewa na:-
UMMY A. MWALIMU (MB)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA,
WAZEE NA WATOTO
DODOMA
09/09/2016