MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imezikamata na kushikilia akaunti za mfanyabiashara maarufu na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza, Anthony Diallo.
Taarifa ambazo gazeti hili limepata mwanzoni mwa wiki hii zinaeleza kwamba TRA imezikamata akaunti hizo kutokana na malimbikizo ya deni linalokadiriwa kufikia shilingi bilioni nne.
Zaidi ya kufahamika kama mwanasiasa, Diallo pia ni mmiliki wa kampuni ya Star Media inayomiliki kituo cha televisheni cha Star Tv na Radio Free Africa.
Hatua hiyo dhidi ya Diallo imekuja katika wiki ambayo Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, naye amekumbwa na mkasa unaofanana na huo.
Wiki iliyopita, Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa kutumia kampuni ya udalali, liliamua kuzishikilia mali za kampuni ya Free Media inayomilikiwa na Mbowe likiwamo klabu ya Bilcanas iliyoko katikati ya jiji la Dar es Salaam kutokana na kumdai Mbowe kiasi cha zaidi ya shilingi bilioni moja.
Akizungumza na Raia Mwema kuhusu taarifa hizo, Kamishina Mkuu wa TRA, Alfayo Kidata, alithibitisha taasisi yake kufungia akaunti za Diallo.
“ Ni kweli kwamba tumezizuia kwa muda akaunti za Diallo. Nimeambiwa na wasaidizi wangu kwamba mfanyabiashara huyo alikuwa anadaiwa fedha nyingi na Mamlaka.
“ Hata hivyo, ifahamike kwamba kuzuia kwetu akaunti za mfanyabiashara huyo au yoyote mwingine haimaanishi kwamba tumefunga mazungumzo. Tunaendelea na mazungumzo kuhusu namna ya kulipa hayo madeni.
“ Ni lazima jamii ituelewe kwamba tunapochukua hatua kama hizi, lengo letu kubwa ni kuona kwamba kila mtu anatimiza wajibu wake. Fedha hizi tunazozidai ni mali ya Watanzania na zikilipwa zitatumika kutatua kero za Watanzania,” alisema.
Kwa upande wake, Diallo alikiri kufungwa kwa akaunti zake lakini akasema hilo si jambo la ajabu kwa mfanyabiashara.
“ Ni kweli kwamba TRA wamefunga akaunti zangu kwa sababu wananidai kiasi cha shilingi bilioni tatu na ushee hivi. Nina mpango wa kuzilipa kupitia makubaliano maalumu nitakayokubaliana na mamlaka hiyo.
“ Hivi unafahamu kwamba wewe ni mbia wa TRA kama ilivyo kwangu. Wewe ni mbia wa Tanesco, Dawasco nk. Hii ni kwa sababu wewe unategemea huduma zao kuendesha maisha yako na wanatarajia wewe utumie na kulipia ili nao waendelee.
“ Mimi nina mali zenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 100. Bilioni tatu na ushee kwangu ni fedha kidogo sana. Nitalipa hizo fedha na maisha yataendelea kama kawaida,” alisema Diallo kwa kujiamini.
Zaidi ya kuwa mfanyabiashara, Diallo aliwahi kuwa waziri, mara ya mwisho akiwa Waziri wa Maliasili na Utalii katika serikali iliyopita ya Rais Jakaya Kikwete na ni mmoja wa wanasiasa mashuhuri hapa nchini.
Wakati tunakwenda mitamboni juzi Jumatatu, benki mbili hapa nchini ziliwasiliana na gazeti hili kudai kwamba nazo ni wadai wa Diallo.
Mara baada ya kukamilika kwa ushahidi wa nyaraka baina ya Diallo na benki hizo mbili, gazeti hili linaweza kuja na habari kamili wiki ijayo.
Tangu kuingia madarakani kwa serikali ya Rais John Magufuli, TRA imeongeza nguvu katika ukusanyaji wake wa mapato na imekuwa ikikusanya wastani wa zaidi ya shilingi trilioni moja katika kipindi cha miezi sita iliyopita.
Katika mazungumzo yake na gazeti hili, Kidata alisema lengo la TRA ni kukusanya mapato kwa kadri inavyowezekana na pia kuhakikisha biashara zilizopo nchini zinaimarika.
“ Ili tukusanye fedha nyingi ni lazima kuwe na mazingira mazuri ya biashara kufanyika. Ndiyo maana, ukiona tunashikilia akaunti za mtu ujue ni kwa lengo la sisi kupata kilicho chetu na si kukomoa kwa sababu zozote zile,” alisema.
Tangu kukamatwa na kushikiliwa kwa mali za Mbowe, kumekuwa na madai ya hatua hiyo kuwa na lengo la kisiasa, lakini kukamatwa huku kwa akaunti za Diallo ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM (NEC) kunaashiria kuwa kila mtu atafikiwa na mkono mrefu wa dola.
Kwa mujibu wa taratibu za TRA, endapo mteja wake atafungiwa akaunti, maana yake ni kwamba hataweza kutumia fedha zote zilizomo kwenye akaunti hiyo.
Chanzo: gazeti la Raia Mwema