Waliobakwa kichawi mkoani Shinyanga waelezea kila kitu

Wakazi wa kijiji cha Nhelegani kata ya Kizumbi katika manispaa ya Shinyanga wameingiwa na hofu baada ya kuibuka mtu asiyejulikana kudaiwa kuwabaka wanawake kishirikina “kufanya mapenzi kimiujiza” baada ya kuwatoa waume zao nje ya nyumba nyakati za usiku na kuiba mali. 



Wakizungumza jana na  Malunde1 blog wanakijiji hao walisema mtu huyo amekuwa akiingia katika nyumba za watu nyakati za usiku wa manane bila wao kujijua kisha kuwaingilia kimwili wanawake bila waume zao kujua.


Baadhi ya wananchi waliofanyiwa vitendo hivyo na mtu au kiumbe hicho ambacho mpaka hivi sasa hawajabaini iwapo ni binadamu au jini walisema hali hiyo imedumu kwa kipindi cha mwezi mmoja hivi sasa.

Walisema mtu huyo huwaibia baadhi ya vitu vya ndani ikiwemo fedha, simu za mkononi, taa aina ya sola na sabuni za kufulia ambapo hata hivyo anapokuta ndani kuna fedha huchukua kiasi na kuachia zingine.


Walisema watu wengi walioingiliwa ndani usiku na mtu au kiumbe huyo mpaka sasa wameshindwa kumfahamu kutokana na kuonekana katika maumbile tofautitofauti ambapo baadhi wanadai huonekana akiwa anatembelea mguu mmoja wenye kwato mfano wa ng’ombe au punda na wengine wakidai ana mguu wa kawaida wa binadamu.

Mmoja wa wanawake waliokumbwa na kadhia ya mtu huyo (jina tunalo) alisema aliingiliwa usiku wa saa nane akiwa amelala ambapo alishitushwa na mtikisiko wa kitanda na kuhisi kuna tetemeko linapita hata hivyo alipojifunua shuka aliona mtu akimmulika kwa mwanga wa simu ya kiganjani akielekea kitandani kwake. 


“Kwa kweli sielewi jinsi gani aliingia ndani, maana hata alipofika kitandani sikujua alivyofika na kuondoa chandarua, ghafla alitoweka, na nilipojikagua nilijiona na hali isiyokuwa ya kawaida, niliogopa sana, na nilishangaa jinsi gani alivyoweza kuingia ndani bila mimi mwenyewe kusikia, alipotoka niliangalia simu yangu sikuiona, ikabidi nitoke nje kuangalia”,aliiambia Malunde1 blog.


“Nilishangaa kukuta mlango uko wazi, na hakuna sehemu yoyote iliyobomolewa, nikaamini anatumia dawa za kishirikina, ilibidi niende kuwagongea jirani zangu na kuwaeleza kilichonitokea, lakini ajabu jirani yangu na mume wake walipoamka pia walishangaa kuona kuna baadhi ya vitu vyao ikiwemo simu zao vimechukuliwa bila wao kufahamu," alieleza mwanamke huyo. 


Mkazi mwingine aliyetoa ushuhuda juu ya sakata hilo (pia jina tunalo)alisema mara nyingi mtu huyo anapoingia ndani akamkuta mwanamke amelala na mume wake, mwanaume huteremshwa kitandani na yeye kulala na mke wake aidha huondoka na mwanamke kimiujiza hadi kwenye eneo la njiapanda ambako humfanyia kitendo kichafu na kumuacha hapo. 


“Ajabu wanawake wanaofanyiwa vitendo vya kuingiliwa kishirikina ni watu wenye umri mkubwa kati ya miaka 40 hadi 45, na anapomaliza kufanya unyama wake huondoka na simu au fedha, na hata anapokuta ndani kuna fedha nyingi huchukua kiasi tu na kuondoka nazo, hachukui zote, sasa hii inatushangaza sana,” alieleza.


Hata hivyo katika jambo la kushangaza baadhi ya viongozi wa walinzi wa jadi sungusungu pamoja na wale wa serikali ya kijiji wanadaiwa kukataa kupeleka taarifa hizo kituo cha polisi na kwamba mtu anayefanya vitendo hivyo anatumia ushirikina na hivyo wao wenyewe wataendesha msako na kuweza kumkamata na kumfikisha polisi.


“Huyu mtu ana miguu miwili,mmoja wa binadamu na mwingine wa punda,akikukuta umelala anamshusha mwanamme kitandani anabaki na mwanamke,au anamtoa mwanamme nje mfano njia panda,asubuhi unajikuta uko nje ,mtu huyo huwa anapuliza dawa mlango unafunguka anaingia ndani bila wewe kujua”,alieleza mhanga mwingine wa tukio hilo.


“Unakuta umelala na mume wako cha kushangaza unamkuta mwanaume wako kalala chini au nje ya nyumba ,mtu huyo anakufanyia mchezo mchafu,lakini pia wakati mwingine milango na madirisha inakuwa imefungwa lakini ukiamka unakuta ipo wazi hakuna sehemu iliyobomolewa na simu zimeibiwa kama sio ushirikina nini jamani?”,alihoji mama mwingine aliyekumbwa na mkasa huo.


Mkazi wa eneo hilo ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema baada ya kuwepo kwa tukio hilo waliwasiliana na mwenyekiti wa kijiji ili suala hilo lichukuliwe hatua kwani wamekuwa wakisikia kuwepo kwa mtu huyo kutoka kwa watu wanaofanyiwa kitendo hicho.

“Tayari inasemekana ameshawaingilia watu watano,huwa anapuliza dawa mlango unafunguka saa nane usiku,huyu mtu hajulikani ni wa aina gani,ukitaka kumkamata anapotea”,aliongeza shuhuda mwingine wa tukio hilo.

Kamanda wa jeshi la jadi (sungusungu) kanda ya Usalala, Nassoro Malaja alikiri kuwepo kwa hali hiyo na kusema kuwa sasa wanaendelea na ulinzi madhubuti na msako mkali kwa ajili ya kumbaini na kumkamata mtuhumiwa huyo.


Mwenyekiti wa kijiji hicho Seni Shija alikiri kupokea taarifa hizo na tayari serikali ya kijiji imekaa kikao ili kutafuta utatuzi , pia amewaomba wananchi hao kuacha kuamini katika nguvu za giza kwani huo ni usumbufu wa vibaka tu.



“Taarifa kuhusu tukio hilo tunazo,tunachukua jitihada za maksusi naomba wananchi wafahamu kuwa tunachukua hatua za haraka,tayari tumeshakaa kikao, ingawa watu wengi wameamini kuwa huu ni uchawi,hii mimi siamini katika ushirikina,mimi ninaamini kuwa kuna vibaka wadogo wadogo tu “,alieleza Shija.


Kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Shinyanga Elias Mwita alisema bado hawajapata taarifa kuhusu tukio hilo.
Na Steve Kanyeph na Kadama Malunde-Malunde1 blog