WANAFUNZI 238 wa shule za msingi na sekondari mkoani Kilimanjaro, wamepewa ujauzito kwa kipindi cha kuanzia Januari hadi Agosti mwaka huu, imeelezwa.
Kutokana na hali hiyo, serikali imewaomba viongozi wa madhehebu ya dini, kusaidia kuokoa baadhi ya wanafunzi hao wa kike waliopewa ujauzito.
Mkuu wa Mkoa huo, Saidi Mecky Sadiki alisema hayo wakati akizungumza na wananchi baada ya kutoa zawadi kwa askari 34 wa Jeshi la Polisi, waliofanya vizuri katika utendaji wao wa kila siku na kudumisha amani na utulivu mkoani hapa.
“Ni fedheha kwa mkoa, kwani tulipowapima wanafunzi Januari hadi Mei mwaka huu mkoa ulikuwa na jumla ya mimba 77... nikaona kuna umuhimu wa kuweka utaratibu maalumu wa marudio, walipopima hadi Agosti zikaongezeka hadi 238,” alisema Sadiki.
Aidha, mkuu wa mkoa alisema kulingana na takwimu hizo, Wilaya ya Rombo inaongoza kwa kuwa na mimba 60 kwa wanafunzi hao kwa kipindi hicho.
“Kwa mwenendo huu kuna haja ya viongozi wa dini kutoa mafundisho maalumu kwa watoto wetu kuepuka vitendo vitakavyochangia wapate ujauzito....hii ni aibu kwa mkoa lakini ni kufuta ndoto za mabinti wetu kuwa wataalam wa fani mbalimbali,” aliongeza.
Alirejea kauli yake ya kutaka viongozi wa mila na utamaduni, kuepuka mila potofu zinazotaka kesi za masuala ya mimba kutatuliwa baada ya pande mbili kupeana jani la sale.
“Zipo mila potofu za kutatua kesi kwa kutoa sale, utamaduni huu haukubaliki, viongozi wa asasi za kiraia na mashirika mbalimbali isaidieni serikali kufichua mila hizo potofu ili hatua za kisheria zichukuliwe kwa wahusika,” alisema.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi wa Mkoa, Wilbrod Mtafungwa alisema kwa kipindi cha Machi hadi Agosti mwaka huu, kumekuwa na matukio 151 ya ubakaji ikilinganishwa na matukio 92 kwa mwaka 2015.
Alisema kwa kipindi kama hicho kwa mwaka 2015, kulikuwa na matukio saba huku mwaka huu tayari kuna matukio 12, matukio manne ya kutupa watoto ikilinganishwa na matukio matatu mwaka 2015.