BODI YA MIKOPO (HESLB) YALAUMIWA KUCHELEWA KUTOA MAJINA YA WANUFAIKA WA MIKOPO

Wakati vyuo vikuu vikikaribia kufunguliwa, Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imelaumiwa kwa kuchelewa kutoa majina ya wanufaika huku yenyewe ikisema itahakikisha majina yanatolewa sanjali na tarehe za vyuo kufunguliwa. 


Pia, HESLB imesema miongoni mwa vipaumbele vitakavyozingatiwa kwenye utoaji wa mikopo katika mwaka wa masomo 2016/2017 ni kwa wanafunzi wenye mahitaji makubwa, waliotoka kwenye kaya masikini, waliosoma shule za kata na waliotoka vijijini. 


Kauli hiyo imekuja baada ya bodi hiyo kutupiwa lawama kwa kuchelewa kutoa majina ya wanufaika wa mikopo kabla hawajaripoti vyuoni, hasa wanafunzi wa mwaka wa kwanza. 


Mkurugenzi wa mtandao wa haki za wanafunzi (TSNP), Shitindi Venance alisema hadi sasa wanafunzi wanaojiunga na masomo ya elimu ya juu nchini kwa mwaka wa kwanza wa masomo 2016/2017, ambao wameomba mkopo bado hawajui ni kiasi gani wamepewa. 


Malalamiko ya Shitindi yamerejea kilichotokea mwaka jana baada ya wanafunzi kuripoti vyuoni, lakini majina yalipotolewa na bodi hiyo baadhi yao hawakuwa wanu- faika hali iliyosababisha usumbufu. 


Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema miongozo ya utoaji wa mikopo kwa wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka huu ni tofauti na mwaka jana. 


“Utaratibu wa mwaka huu ni tofauti kwa kuzingatia wanafunzi wanaoanza masomo na wale wanaoendelea na masomo katika vyuo mbalimbali,” alisema Badru. 


Mkurugenzi huyo alibainisha kuwa majina ya wanufaika wa mikopo yataanza kutolewa kwa kuzingatia tarehe ambayo chuo husika kinafunguliwa. 


“Kila chuo kinafunguliwa kwa mujibu wa tarehe iliyopangwa kwa hiyo na sisi tunatoa majina kuendana na utaratibu wa chuo husika,” alisema. 


Hata hivyo, Badru alisema uta- ratibu wa kupanga viwango vya mikopo kwa wanafunzi na kisha kutoa orodha ya majina ya wanufaika haihusishi bodi ya mikopo peke yake. 


Alisema kabla ya kuidhinisha majina ya wanufaika na mikopo, lazima Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) iwe imeshatoa orodha ya majina wa wanafunzi ambao imewadahili kwa kuzingatia vigezo vyao, halafu majina hayo yatumwe vyuoni. 


Alisema mzunguko wote huo unahitaji muda na umakini wa hali ya juu ndiyo maana huchukua muda.