KIAMA CHA WENYE VYETI FEKI: NECTA KUANZIA KESHO KUTUA HADI MAENEO YA VITUO VYA KAZI,HIII HAPA RATIBA YA UHAKIKI

Hatua ya Baraza la Mitihani nchini (Necta) kutoa ratiba ya kufanya uhakiki wa vyeti vya kidato cha nne, sita na ualimu kwa watumishi wote wa umma sasa ni wazi imezidi kupandisha joto kwa vigogo na watumishi mbalimbali ambao hawana sifa za kielimu kushika nafasi walizo nazo.


Katika taarifa yake ya sasa Baraza la Mitihani nchini, limetangaza kuwafuata katika maeneo yao ya kazi watumishi wote walioko katika mamlaka za mikoa, halmashauri na manispaa kwa ajili ya kufanya uhakiki wa vyeti vyao hivyo vya kitaaluma. 


Kwa mujibu wa barua iliyosainiwa na Edga Kasuga kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Baraza hilo kwenda kwa Makatibu tawala wa Mikoa, uhakiki utafanyika katika ofisi za Makatibu Tawala wa mikoa kuanzia Oktoba 10 hadi 14 mwaka huu, ingawa ratiba nyingine ya uhakiki imeonyesha zoezi hilo litafikia tamati Novemba 7 mwaka huu. 


“Ili kufanikisha zoezi hilo Baraza limetaka kupata orodha (nakala- laini ya soft copy) ya watumishi wote wa umma waliopo katika Mkoa, Halmashauri na Manispaa. 


“Nakala za vyeti vya kidato cha nne, cha sita na ualimu vya watumishi wote walioandikishwa na chumba cha kufanyia uhakiki,” inaeleza taarifa hiyo ya Baraza la Mitihani. 


Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Baraza la Mitihani, uhakiki huo utafanywa katika makundi matano katika mikoa tofauti tofauti. 


Oktoba 10, mwaka huu kundi la kwanza litafanya uhakiki katika Mkoa wa Mtwara, kundi la pili Singida, kundi la tatu Rukwa, kundi la nne Katavi na kundi la tano litakuwa Geita. 


Oktoba 17 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa Lindi, la pili Manyara la tatu Songwe, la nne Kigoma na la tano litakuwa Mwanza. 


Oktoba 24 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa Morogoro, la pili Arusha, la tatu Mbeya, la nne Tabora na la tano Mara. 


Oktoba 31 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa Pwani, la pili Kilimanjaro, tatu Ruvuma, la nne Shinyanga na la tano Simiyu. 


Novemba 7 mwaka huu, kundi la kwanza litakuwa Dar es Salaam, la pili Tanga, la tatu Njombe, la nne Dodoma na la tano Iringa.
==