Mwanamke aliyemnyofoa ulimi mwanaume wakati wakila denda afikishwa Mahakamani

Mwanamke anayedaiwa kumng’ata ulimi kijana Saidi Mnyambi (26) siku 28 zilizopita, kwa kile kilichodaiwa kutaka kufanya naye mapenzi kwa nguvu, hatimaye amefikishwa katika Mahakama ya wilaya ya Singida.


Mwanamke huyo, Mwajabu Jumanne (36) mkazi wa eneo la Mandewa nje kidogo ya mji huu amefikishwa mbele ya Hakimu Flora Ndale akishitakiwa kwa kosa la kujeruhi kwa kunyofoa theluthi moja ya ulimi wa kijana Mnyambi wakati wakipeana denda.
Wakili wa Serikali, Michael Ng’hoboko alidai mbele ya hakimu Ndale kuwa Septemba 12 mwaka huu majira ya saa 2.45 usiku katika eneo la Mandewa Manispaa ya Singida, kwa makusudi, mama huyo alimng’ata ulimi Mnyambi na kumsababishia jeraha na maumivu makali.
Mwendesha mashitaka huyo alidai kuwa mshitakiwa Mwajabu alitenda kosa hilo kinyume na kifungu namba 225 cha Kanuni ya adhabu Sura ya 16 Sheria za nchi kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.
Mshitakiwa alikana kosa na kesi hiyo iliahirishwa hadi Oktoba 24 itakapotajwa tena.
Mshitakiwa yupo nje kwa dhamana ya watu wawili waliotoa ahadi ya Sh milioni moja kila mmoja.