BODI YA MIKOPO YATANGAZA SIKU 90 KWA WAOMBAJI WA MIKOPO ELIMU YA JUU KUKATA RUFAA


Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) imetangaza siku 90 kuanzia jana (Jumatatu, Oktoba 31, 2016) kwa waombaji wa mikopo kwa mwaka wa masomo 2016/2017 kukata rufaa kwa njia ya mtandao ikiwa hawajaridhishwa na matokeo ya upangaji uliotangazwa hivi karibuni. 

Serikali imetenga Tshs 483 bilioni kwa ajili ya kutoa mikopo kwa jumla wanafunzi 119,012 – kati yao, wanafunzi 93,295 ni wanaondelea na masomo na wanafunzi 25,717 ni wa mwaka wa kwanza. Hadi sasa, jumla ya wanafunzi 20,183 wa mwaka wa kwanza wameshapata mikopo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana (Jumatatu, Oktoba 31, 2016) na Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB Bw. Abdul-Razaq Badru, Bodi imeanza kupokea rufaa hizo kwa njia ya mtandao (Online Loan Application and Management System) kuanzia leo (Oktoba 31, 2016) hadi Januari 31, 2017.

“Wanachotakiwa kufanya wanafunzi ni kuingia katika mtandao wetu wahttp://olas.heslb.go.tz na kujaza fomu, kuichapa na kuiwasilisha kwa Afisa Mikopo wa chuo chake ambaye atawasilisha kwetu fomu zote za chuo chake kwa barua kwa ajili ya sisi kuzifanyia kazi,” amesema Bw. Badru.

ANGALIZO: Ada ya Maombi ya Tshs 10,000/- iliyopaswa kulipwa na waombaji mikopo kwa MPesa kwa ajili ya malipo ya Rufaa (HESLB) imefutwa.Taratibu nyingine zinabaki palepale