Kijana mmoja nchini Afrika Kusini, Victor Mlotshwa amelazimishwa na wanaume wawili wazungu kuingia ndani ya jeneza na kisha akarekodiwa video ambayo imeibua hisia tofauti miongoni mwa watazamaji.
Akizungumzia tukio hilo, Victor alisema kuwa alikuwa akitembea wakati tukio hilo lilipotokea. Alisema kuwa kulikuwa kuna njia ya waenda kwa miguu na akaamua kuitumia. Alipokuwa akipita katika barabara hiyo alifika mahali akakuta jeneza na kaburi limechimbwa.
Ghafla wazungu wawili walimtuhumu kupita katika eneo la ranchi bila ya kuwa na kibali. Baada ya kumkamata walimlazimisha kijana huyo kuingia ndani ya jeneza lililokuwa pembeni. Lakini pia ameeleza kuwa walimtishia kumchoma moto huku mmoja wa waliomkamata akimrekodi wakati akilazimishwa kuingia kwenye jeneza.
Video hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii inamuonyesha mzungu huyo akijaribu kulifunika jeneza wakati Victor akikazana kumzuia asifanye hivyo. Video hiyo haikuonyesha hadi mwisho ni kitu gani kilitokea.
Watuhumiwa hao wawili Willem Oosthuizen na Theo Martins Jackson wamefikishwa mahakamani leo wakikabiliwa na mashtaka mawili ya kuteka na kutaka kujeruhi. Watuhumiwa hao walipelekwa rumande na kesi hiyo itanendelea tena Januari mwakani.
Victor Rethabile Mlotshwa (C) akisindikizwa baada ya kutoka mahakamani leo nchini Afrika Kusini.
Mamia ya waliojitokeza mahakamani leo wamesema kuwa sababu pekee iliyopelekea Victor kufanyiwa ukatili huo ni kwa sababu ni mweusi.