Mkuu wa wilaya asema hali ya Uchumi ni mbaya katika wilaya yake

Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, amesema hali ya uchumi kwa baadhi ya vijana na kina mama katika wilaya hiyo ni mbaya kutokana na matumizi mabaya ya fedha hali ambayo inawarudisha nyuma kiuchumi.


Ameyasema hayo kwenye mahojiano maalum na East Afrika Radio ilipotaka kujua uongozi wa wilaya hiyo inafanya jitihada gani katika kuhakikisha inawainua kiuchumi vijana na kina mama ambao wamekua wakilalamika kukosa mitaji ya kufanya biashara ambazo zitawainua kimaisha na kuwapatia vipato vyao vya kila siku.

Amesema wametengeneza mikakati ya kuwaongoza katika kufanya matumizi na kuwapa mafunzo ya mifumo maalumu ya utunzaji wa fedha ili kuwapa ujasiri wa kutoogopa kukopa fedha za kuendesha biashara zao, kutoka kwenye taasisi mbalimbali za kibenki sambamba na hilo wawe na uthubutu wa kujitafutia mitaji.

Aidha ameongeza kuwa tayari ameanza mazungumzo na wamiliki wa viwanda mbalimbali nchini ili kuhakikisha bidhaa zinazolimwa katika wilaya hiyo zinapata soko la kimataifa, sambamba na hilo watahakikisha bidhaa za vyakula zinazozalishwa nchini zinatokana na mazao yanayolimwa katika wilaya ya Iringa.


Wakati huohuo amewataka wananchi wa wilaya hiyo kushirikiana kwa pamoja katika kuhakikisha wanasimamia malengo yao waliojiwekea yanatimia kwa wakati na kuachana na itikadi zao na kwa yule atakayezuia maendeleo ya eneo hilo atachukuliwa hatua za kisheria.