Siku chache tu baada ya viungo vya mwili wa mtoto mchanga kudaiwa kuzagaa mtaani, jeshi la polisi mkoani Shinyanga linamshikilia msichana aliyejulikana kwa jina la Elizabeth Benjamin (20) anayedaiwa kutoa mimba ya miezi minane na kisha kufukia mwili wa mtoto.
Kaimu Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani hapa Elias Mwita amethibitisha kukamatwa kwa msichana huyo Septemba 9, mwaka huu.
Mwita alisema baada ya jeshi hilo kupata taarifa kutoka kwa raia wema,askari walimkamata nyumbani kwake mtaa wa Butengwa, Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga.
Alisema katika mahojiano msichana huyo alikiri kufanya kitendo hicho na kueleza kuwa katika maelezo ya awali, msichana huyo alieleza kuwa yeye ni mfanyakazi wa baa iliyopo mjini Shinyanga.
Aliongeza kuwa bado wanaendelea na mahojiano na baada ya kukamilika, watamfikisha mahakamani kujibu mashtaka yanayomkabili.
Wakazi wa mtaa huo walieleza kuwa baada ya tukio kutokea hawakufahamu aliyehusika na unyama huo.
Lakini baada ya siku moja kupita walishangaa kuona askari wakifika kwenye nyumba anayoishi msichana huo, aliyefika hapo kumtembelea dada yake, ambapo katika mahojiano alikiri kutoa mimba ya miezi sita na kufukia mtoto nje kidogo ya nyumba hiyo.
“Sisi tulishangaa kuona msichana huyo anaongoza moja kwa moja akiwa ameambatana na askari eneo ambalo anadai ndiyo alizika kiumbe hicho, wakajiridhisha na kumuona hali yake ilivyo kisha wakaondoka naye kwenda kituoni, lakini dada yake alikuwa akikataa kuwa ndugu yake siyo mhusika wa tukio hilo",walisema.
Mwenyekiti wa Mtaa huo Juma Derefa alisema msichana aliyetupa mtoto na viungo vyake kuzagaa hovyo mitaani, amepatikana na tayari anashikiliwa na jeshi la polisi, ambapo lilibaini kuwa alikuwa ni mjamzito.