POLISI mkoani Rukwa inamshikilia mkazi wa eneo la Majengo Manispaa ya Sumbawanga, Rose Mwananzumi, akituhumiwa kumtendea unyama mtoto wake mwenye umri wa miaka sita, kwa kumpiga na kumchoma kwa kisu cha moto na kumsababishia majeraha makubwa mwilini.
Mtoto huyo anasoma darasa la kwanza katika Shule ya Msingi Majengo katika Manispaa ya Sumbawanga.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alisema mama huyo anatuhumiwa kutenda unyama huo Septemba 4, mwaka huu, usiku katika eneo hilo.
Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Majengo, Losko Manase alisema juzi kuwa wanafunzi wenzake walimgundua mtoto huyo (jina linahifadhiwa) akiwa na majeraha makubwa mwilini ndipo wakatoa taarifa kwa walimu.
“Mtoto huyo alituonesha majeraha ya moto mikononi, miguuni, mgongoni na tumboni …. Tulipomhoji alisema mama yake mzazi alimwadhibu kwa kumchoma kwa kisu chenye moto …. ndipo tukamtaarifu Ofisa Mtendaji ili askari mgambo wamkamate mama huyo,” alieleza Mwalimu Mkuu.
Ofisa Mtendaji Kata ya Majengo, Lucy Mwakyusa alikiri kupokea taarifa ya mkasa huo kutoka kwa Mwalimu Mkuu wa Majengo, na alichukua hatua ya kumkamata na kumfikisha kwenye vyombo vya dola.
Akizungumzia mkasa huo, mtoto huo huku akionesha majeraha katika sehemu mbalimbali za mwili, alisema siku hiyo ya tukio hakushinda nyumbani alikuwa akichunga ng’ombe za jirani yao ambapo alirejea nyumbani jioni alitendewa vitendo hivyo.