VIONGOZI WA UKAWA WAKUTANA OFISINI KWA LOWASSA

Siku moja baada ya aliyekuwa mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba kuwasimanga viongozi wa Ukawa kuhusu namna walivyompokea Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa na kumteua kuwa mgombea urais, viongozi hao jana walikutana katika kikao kilichotarajiwa kujadili suala hilo.

Kikao hicho cha Ukawa kimekuja zikiwa zimepita siku nne baada ya Lowassa na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kukutana nyumbani kwa Lowassa Jumatatu ya wiki hii.

Juzi, katika mahojiano na kituo cha redio cha Clouds FM, Profesa Lipumba alisema mkutano wa chama hicho ulioridhia Lowassa kuingia Ukawa ulifanyika Zanzibar bila yeye kuambiwa, kitendo kinachoonyesha kuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alikuwa akimzunguka.

Mbali na tuhuma hizo, kiongozi huyo alieleza kuwa hatakuwa tayari kuona CUF ikinunuliwa kwa bei chee na Lowassa au Chadema hata kama atakuwa nje ya chama hicho.

Jana jioni, viongozi wa vyama hivyo walikutana faragha kwenye ofisi za Lowassa zilizopo Mikocheni. Haikuweza kufahamika mara moja ajenda za kikao hicho lakini habari kutoka ndani ya vyama hivyo zilisema pamoja na mambo mengine kilitarajia kujadili shutuma zilizotolewa na Profesa Lipumba.

Suala jingine lililotarajiwa kujadiliwa na viongozi hao washirika wa Ukawa ni mkakati wa pamoja wa namna ya kuendesha shughuli za siasa katika kipindi ambacho imetolewa amri ya kuzuia maandamano na mikutano ya siasa.

Baadhi ya viongozi waliohudhuria kikao hicho ni mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru aliyewasili saa 10.56 jioni, Mwenyekiti wa Ukuta Profesa Mwesiga Baregu aliyewasili saa 11.06 akafuatiwa na Maalim Seif saa 11.13, na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe saa 11.18 jioni.

Mbali na kikao hicho, viongozi mbalimbali wa CUF, walijitokeza kumjibu Profesa Lipumba aliyejiuzulu uenyekiti katika kipindi cha mapambano ya kukiondoa madarakani chama tawala, CCM, lakini kauli ya pamoja ya viongozi hao ndiyo inasubiriwa kukata mzizi wa fitina.

Juzi, Naibu Katibu Mkuu wa CUF Zanzibar, Nassor Ahmed Mazrui alisema Profesa Lipumba ni “kigeugeu” huku Mbowe akisema “hakutegemea maneno hayo yangetoka kwa mtu kama Profesa Lipumba.”

Jana asubuhi akitumia kituo cha Clouds FM, Kaimu Naibu Mkurugenzi wa Habari, Uenezi na Mahusiano wa CUF, Mbarara Maharagande alisema siyo kweli kwamba Profesa Lipumba hakushirikishwa katika ujio wa Lowassa bali yeye ndiye aliyepeleka taarifa katika Baraza Kuu la chama kwamba Ukawa wamekubaliana kumsimamisha Lowassa.

“Alichokuwa anakifanya Maalim Seif ni haki yake kikatiba kushirikiana na viongozi wengine wa Ukawa. Mbona yeye alikwenda kumfuata Mzee Joseph Warioba kumshawishi agombee urais?” alihoji.

Maharagande alisema CUF walimtazama Lowassa kama sura ya kuleta mabadiliko kwa yale waliyokuwa wakiyataka katika Ukawa. 

“Profesa Lipumba alimtazama Lowassa kama mtu wa kawaida, lakini CUF walimtazama kama kiongozi mwenye ushawishi mkubwa kwa sababu ya uwezo wake wa kuunganisha wanasiasa,” alisema.

Pia, jana mchana Mwanasheria wa Chadema, Tundu Lissu alisema Profesa Lipumba ambaye ni msomi ameanguka kifikra kutokana na kauli zake na ukweli uliopo.

Lissu, ambaye ni Mbunge wa Singida Mashariki alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa swali na waaandishi wa habari katika mkutano wake jana waliotaka kujua msimamo wake kutokana na matamshi aliyoyatoa Profesa Lipumba.

“Kwa kifupi ya Profesa Lipumba yasiwasumbue CUF na wala Chadema hayatusumbui. Wanaosumbuka ni wale wanaomtumia Profesa, kwa sababu ukweli uko wazi kutokana na mambo yaliyojitokeza baada ya ujio wa Lowassa,” alisema Lissu.

Alisema katika chaguzi zote ambazo Profesa Lipumba alikuwa akigombea urais, CUF Bara haikuwahi kupata viti vya ubunge zaidi ya viwili lakini mwaka jana kimepata viti 10 kutokana na ushirikiano wa Ukawa.

Lissu aliwahi kumwelezea Lowassa kuwa pamoja na shutuma nyingi anazorushiwa nchini bado ni tembo katika uwanja wa siasa ambaye “ukifumba macho yupo, ukisema hayupo, yupo pale.”

Lowassa kama “jongoo mpenda watu na watu hawampendi” alisababisha zogo kubwa ndani ya CCM wakati wa mchakato wa kuteua mgombea urais na jina lake lilipokatwa aliamua kutulia.

Kutokana na ushawishi mkubwa alionao katika jamii, Chadema walimfuata kumwomba ajiunge nao na akateuliwa kuwa mgombea urais na baadaye alinadiwa kwa vyama vinavyounda Ukawa vya CUF, NCCR-Mageuzi chini ya James Mbatia na NLD chini ya hayati Dk Emmanuel Makaidi.