Bondia Thomas Mashali, ameuawa kwa kupigwa na wananchi wenye hasira usiku wa kuamkia leo, baada ya kupigiwa kelele za mwizi kufuatia ugomvi uliozuka maeneo ya Kimara, jijini Dar es Salaam.
Bondia, Francis Miyeyusho aliyekuwa mwanafunzi wake, ameiambia East Africa Radio kuwa Mashali aliumizwa vibaya kichwani. Amesema Jumapili hadi saa tisa alasiri walikuwa pamoja kwenye kikao cha masuala ya masumbwi na alimuaga kuwa anaenda Kimara.
“Baadaye nikaja kusikia story kwamba kuna mtu kagombana naye pale wamemchenjia wameanza kumuitia kelele za mwizi mitaa ya Kimara huko kwahiyo wamemchangia raia, wamempiga,” amesimulia Miyeyusho.
Bondia huyo amesema kuwa Mashali alikuwa amenyoa rasta zake na kwamba huenda hiyo ni sababu wananchi wengi walishindwa kumtambua.
Kwa upande wa baba yake mzazi, Mzee Christopher Mashali, amesema alipata taarifa hizo usiku akiwa amelala kutoka kwa vijana wanaomfahamu. Vijana hao walimweleza kuwa mtoto wake amepigwa vibaya kiasi cha kupasuliwa kichwa na usiku huo kuwapigia simu wanae wengine waliopo Dar.
Anasema Mashali alifariki Muhimbili kutokana na kuwa amejeruhiwa mno ikiwa ni pamoja na kutolewa ubongo. Mzee Mashali anasema mara ya mwisho kuwasiliana na mwanae ilikuwa jana (Jumapili) mchana.
“Alinitumia meseji ambayo bado ninayo hapa akaniambia ‘baba nipo kwenye kikao, nikimaliza kikao nitakujibu baba’ ndio mara ya mwisho nimewasiliana naye,” ameeleza mzee huyo.
Amesema kinachoendelea sasa ni kupata ripoti ya polisi, kupewa ruhusa ya kuuchukua mwili wa marehemu tayari kwa mazishi.
Mashali aliyezaliwa mwaka 1980, ameacha watoto watano.