Kwa wasichana wengi wanaoshiriki shindano la Miss Tanzania, ushindi huja kwa surprise na muda mfupi kugubikwa na matarajio makubwa kutoka kwenye jamii.
Lakini si kwa Miss Tanzania 2016, Diana Edward aliyevishwa taji Jumamosi hii, jijini Mwanza. Tangu ameanza kushiriki shindano hilo katika hatua za vitongoji, mrembo huyo alikuwa amejianda kuwa Miss Tanzania.
Diana mwenye asili ya kimasai, kwa muda wote wa ushiriki wa shindano hilo, aliuweka mbele utamaduni wake, kitu ambacho ni nadra kwa Mamiss wengine ambao wengi wao wamekulia mjini.
Amekuwa akijihusisha na shughuli za utetezi wa masuala ya kijamii, hasa watu wanaoishi mazingira magumu, pamoja na kampeni za kutokemeza ukeketaji. Wiki moja iliyopita alitoa documentary fupi kuhusu ukeketaji unaofanyika katika jamii yake ya kimasai. Yeye mwenyewe ni mhusika.
Diana Edward Loi Lukumay ana umri wa miaka 18 tu. Alizaliwa mwaka 1998 katika hospitali ya Mount Meru, Arusha. Ni mtoto wa tatu katika familia ya watoto wanne.
Elimu yake ya msingi aliipata katika shule Levolosi, 2005-2011, alisomea shule ya sekondari Arusha Mwaka, 2012-2015 na kupata daraja la pili kwenye mtihani wa kidato cha nne.
“Nilichaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha tano mchepuo wa Sanaa kwenda shule ya Wasichana ya Bwiru iliyopo jijini Mwanza,lakini kwakuwa nilikuwa tayari nipo katika tasnia hii ya urembo niliamua kutojiunga na masomo hayo kwakuwa tayari yalikuwa yameingiliana na ratiba za mashindano haya katika ngazi ya vitongoji,ambapo nilijiunga na Kambi ya Miss Ubungo 2016/2017 ambapo nilishika nafasi ya tatu nakutunukiwa taji la Miss mwenye kipaji (Ubungo Miss Talent 2016/2017),” Diana amejielezea.
“Baada ya kuahirisha masomo ya kidato cha tano niliomba kujiunga na masomo ngazi ya cheti kozi ya maswala ya kodi katika Chuo cha Usimamizi wa fedha (IFM) ambapo mpaka masomo yanaanza mwanzoni mwa mwezi wa Oktoba tayari nilikuwa kwenye kambi ya Miss Tanzania.”
“Nilipotangazwa mshindi sikubweteka na taji hilo la Miss Kinondoni bali niliendelea na kazi zangu za kijamii katika jamii yangu ya kimasai.”
Kwa msingi aliojiwekea Diana tangu mwanzo kabisa, ana nafasi kubwa ya kuja kufanya vizuri kwenye shindano la Miss World.