KAKA AMPASUA KICHWA KWA PANGA MDOGO WAKE WAKIGOMBANIA FEDHA

MKAZI wa kijiji cha Ntalamila kata ya Miyula wilayani Nkasi mkoani Rukwa, Baraka Kaengele (23) ameuawa kikatili na kaka yake wa tumbo moja, Edward Kaengele (25) kwa kumshambulia na kumpasua kichwa kwa panga na ubongo kutokeza nje. 


Inadaiwa wanandugu hao walihitilafiana wakati wakigawana fedha, walizolipwa baada ya kumaliza kufanya kazi za vibarua shambani. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, George Kyando alidai tukio hilo lilitokea Oktoba 27, mwaka huu saa mbili na nusu usiku katika kijiji cha Ntalamila kilichopo kata ya Miyula, wilayani Nkasi. 

“Chanzo cha mauaji ni ugomvi wa kifamilia ambapo ndugu hawa wa familia moja walikuwa wakigombania fedha walizolipwa baada ya kufanya kazi za vibarua katika mashamba,” alieleza Kamanda Kyando. 

Akisimulia mkasa huo, Kamanda Kyando alisema siku hiyo ya tukio, ndugu hao walikuwa kilabuni wakinywa pombe ya kienyeji kijijini humo, ndipo ugomvi uliibuka baina yao baada ya kuhitilafiana wakati walipokuwa wakigawana fedha walizolipwa baada ya kumaliza kufanya kazi, ingawa hadi sasa kiasi hicho cha fedha hakijajulikana. 

“Baada ya kuibuka ugomvi huo, ndipo kaka wa marehemu alipompiga mdogo wake kichwani na kumpasua fuvu na kumsababishia umauti,” alieleza Kamanda Kyando na kuongeza kuwa mtuhumiwa amekamatwa na atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi wa shauri lake kukamilika.
               KWA HABARI ZA VIJANA INGIA HAPA!!!