Mama, wanaye wanne wafa kwa kula chakula chenye sumu

Mama na watoto wake wanne wamefariki dunia jana katika Kijiji cha Nyamilanda, Muleba mkoani Kagera, baada ya kula ugali unaosadikiwa kuwa na sumu.

Kaimu mwenyekiti wa kijiji hicho, Trasias Baltromeo alisema kabla ya vifo hivyo, mama huyo na watoto wake walikula ugali saa tisa alasiri na kuanza kutapika na walifariki dunia walipokuwa wakipelekwa Kituo cha Afya Kimeya, kilichoko jirani na kijiji hicho.

Waliofariki ni Julitha Julius (35) na watoto wake Haujeni Julius (14) Superius Julius (12), Gabriel Julius (4) na Paschazia Julius mwenye umri wa miezi sita.

Awali, mama huyo alipika dagaa na kwenda kwa mama mkwe wake jirani na kupewa unga wa muhogo kwa ajili ya ugali na baada ya kula walianza kutapika na kuhangaika. Jitihada za majirani kuokoa maisha yao hazikuzaa matunda.

 “Nilipofika nilikuta hali ni mbaya wakitapika. Nikatoa taarifa Polisi Kyebitembe lakini walipofika wakati wanawapeleka hospitali ya Kimeya wakawa wamefariki watoto wawili na mama yao,” alisema Baltromeo.

Mkuu wa Wilaya ya Muleba, Richard Ruyango alisema jopo la wataalamu wa afya na Jeshi la Polisi walikwenda Kituo cha Afya Kaigara na Hospitali ya Rubya kufanya uchunguzi.

Alisema baada ya uchunguzi, ilibainika kwamba walikula chakula chenye sumu lakini haikujulikana ni ya aina gani, hivyo sampuli imepelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Dar es Salaam.

Mkuu huyo wa wilaya ameonya kuongezeka kwa matukio ya vifo vinavyotokana na kula sumu katika Tarafa ya Kimwani.

Ruyango alisema jeshi la polisi na kamati za ulinzi na usalama za kijiji na kata zimepewa jukumu la kufanya uchunguzi na kubaini wanaohusika ili hatua za kisheria kwani zichukuliwe.

Mwaka jana, katika Kata ya Kasharunga, watu saba wa familia moja walikula chakula chenye sumu na wanne kufariki dunia.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera, Agustino Olomi alisema hakuna anayeshikiliwa kwa matukio hayo na uchunguzi wa wataalamu wa afya unaendelea ili kujiridhisha na kutambua aina ya sumu iliyotumika.