Marekani Yaufunga Ubalozi Wake Nairobi

NAIROBI, KENYA: Nchi ya Marekani imeamua kuufunga kwa muda ubalozi wake uliyopo jijini Nairobi nchini Kenya leo Ijumaa, Oktoba 28, 2016 kufuatia kisa ambapo mwanamume aliyekuwa na kisu alijaribu kumshambulia afisa wa usalama karibu na ubalozi huo jana Alhamisi.

Imearifiwa kuwa mwanamume huyo aliuawa kwa kupigwa risasi na hakuna afisa yeyote wa ubalozi huo aliyeathiriwa na kisa hicho.
“Ubalozi utafungwa Oktoba 28. Huduma zote za kibalozi zimesitishwa, lakini huduma za kibalozi za dharura kwa raia wa Marekani zitaendelea kutolewa,” Taarifa hiyo imetolewa kwenye tovuti ya ubalozi huo.
Maafisa wa ubalozi huo wametoa wito kwa raia na wafanyakazi wake kuwa makini kuhusu usalama wao.
Polisi nchini Kenya wanachunguza kubaini iwapo mwanamume huyo aliyepigwa risasi alikuwa na washirika, afisa mmoja mkuu wa polisi Vitalis Otieno aliambia Shirika la Habari la AFP.
Bw Otieno alisema mwanamume huyo alimdunga kisu afisa mmoja wa polisi lakini akapigwa risasi na kichwani na kuuawa na afisa aliyekuwa karibu.
Maafisa watano wa idara ya uchunguzi wa jinai ya Marekani (FBI) walifika eneo la tukio muda mfupi baadaye pamoja na polisi wa Kenya kufanya uchunguzi.
Msemaji wa polisi Kenya George Kinoti alisema mwanamume huyo wa miaka 24 alikuwa “mhalifu wa kuendesha shughuli zake kivyake”, kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters.
Hata hivyo, alisema uchunguzi unaendelea.