UONGOZI wa kampuni ya DIRA NEWSPAPER COMPANY LTD wachapishaji wa gazeti DIRA YA MTANZANIA unamwomba radhi Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi na Usalama wa nchi na jeshi la wananchi wa Tanzania kwa ujumla kwa habari iliyochapishwa kwa bahati mbaya katika gazeti letu; toleo Na.424 la Juni,20-26 ,2016 iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho “KIFARU CHA KIVITA CHA JWTZ CHAIBWA”.
Tunapenda kueleza kwa masikitiko kuwa habari hiyo ilichapishwa kwa bahati mbaya baada ya mtayarishaji wa kurasa (graphic designer) kuipanga habari ambayo ilikuwa haijakamilika kiuchunguzi na kuiacha iliyotakiwa ichapishwe siku hiyo.
Tunapenda JWTZ na watanzania wote kwa ujumla kuwa wafahamu kuwa gazeti la DIRA YA MTANZANIA halikulenga kuchafua Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kama ambavyo baadhi ya watu walivyofikiria.
Tunafahamu mchango mkubwa wa jeshi la wananchi wa Tanzania kwa taifa letu na namna jeshi hilo linavyoshirikiana kwa kiasi kikubwa na vyombo vya habari hasa utoaji wa taarifa mbalimbali na kamwe jeshi hili tokea kuanzishwa kwake halijawahi kukwaruzana na vyombo vya habari jambo ambalo ni heshima kubwa kwetu na taifa kwa ujumla.
Hivyo uongozi wa gazeti hili umeonelea kuomba radhi kwa Mkuu wa majeshi (CDF), askari wote wa JWTZ na watanzania wote walioshitushwa na habari hiyo na hasa mkuu wa kikosi cha 83 KJ cha Kiluvya mkoani Pwani ambaye kikosi chake kilitajwa kama chanzo cha habari hiyo.
Na tunaomba ifahamike kuwa tumeomba radhi kwa ridhaa yetu na tunaamini kuwa “kuomba radhi” ni kitendo cha kiungwana kwa utamaduni wa waafrika na hasa watanzania tuliokulia katika misingi ya amani, upendo na utulivu na pia tunaamini kuomba kwetu radhi kutazidisha mahusiano mema na ya karibu kati yetu na JWTZ.
Tunatanguliza shukrani zetu.