Samatta Atokea Benchi Genk Ikiua 2-1 Ubelgiji

MSHAMBULIAJI wa kimataifa wa Tanzania, Mbwana Ally Samatta amecheza benchi timu yake, KRC Genk ikishinda 2-1 dhidi ya Westerlo katika mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza A Ubelgiji, Uwanja wa Laminus Arena.

Kiungo Mspaniola, Alejandro Pozuelo aliifungia bao la kwanza Genk dakika ya 54 kabla ya mshambuliaji Mgiriki, Nikolaos Karelis kufunga la pili dakika ya 66, wote wakimalizia pasi za mshambuliaji Mjamaica, Leon Bailey.

Na ni Nikolaos Karelis aliyempisha Samatta, Nahodha wa timu ya taifa ya Tanzania 'Taifa Stars' dakika ya 66 mara tu baada ya kufunga bao la pili. Bao pekee la wageni lilifungwa na kiungo Mbelgiji, Jamo Molenberghs dakika ya 82.

Huo unakuwa mchezo wa 31 kwa Samatta tangu amejiunga na Genk Januari mwaka huu kutoka TP Mazembe ya DRC, 18 msimu uliopita na 12 msimu huu, akifunga mabao nane, matatu msimu huu na matano msimu uliopita.

Katika mechi hizo, ni 16 tu ndiyo alianza, 10 msimu uliopita na tano msimu huu, wakati 14 alitokea benchi nane msimu uliopita na 11 msimu huu – na mechi tisa hakumaliza akitolewa, sita msimu uliopita na tatu msimu huu.