Sumaye Adai Amepata Taarifa ya Kutimuliwa Nyumbani kwake pia

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Serikali ya Awamu ya Tatu, Frederick Sumaye amesema kuwa baada ya kutangazwa mchakato wa kunyang’anywa shamba lake la Mwabwepande, amepata taarifa ya kutaka kuondolewa anapoishi pia.

Sumaye ametoa kauli hiyo ikiwa ni siku chache baada ya Waziri Wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi kueleza kuhusu kuanza rasmi kwa mchakato wa kumnyang’anya mwanasiasa huyo shamba la Mwabwepande kwa madai ya kutoliendeleza kwa muda mrefu.

“Hapa ninapoishi naambiwa kuna maelekezo yametoka juu kuwa sijapaendeleza. Sasa kama sijapaendeleza mbona ninaishi hapahapa,” Sumaye amekaririwa na gazeti la Nipashe.

Aidha Sumaye amesema kuwa ingawa alimsikia Waziri Lukuvi akieleza kuwa tayari wameshampa notisi ya siku 90 kuhusu kunyang’anywa shamba lake la Mwambwepande, hadi jana hajaipata notisi hiyo licha ya kufanya jitihada za kuifuatilia.

Alisema kuwa anashangazwa na uamuzi huo wa Waziri kwani kesi inayolihusu shamba hilo bado inaendelea mahakamani kutokana na uvamizi wa wananchi na kwamba Mahakama imezitaka pande zote mbili kutofanya chochote kwenye ardhi hiyo.

Mwanasiasa huyo ambaye pia ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chadema alisema kuwa anachokifahamu ni kwamba alipokea notisi ya kuondolewa katika shamba lake la Mvomelo kwa madai ya kushindwa kuliendeleza kwa muda mrefu.

“Ninachokijua ninaandamwa kisiasa. Shamba langu la Mvumelo naambiwa sijaliendeleza. Kwenye hilo shamba nimejenga nyumba ya kuishi, ghala, kuna trekta na vifaa vingine. Ninalima mazao na nimefuga zaidi ya ng’ombe 200, nina kondoo 300 na nimechimba visima viwili vya maji halafu serikali inasema sijaliendeleza,” alisema Sumaye.

Alisisitiza kuwa ingawa anaamini anaandamwa kisiasa kwa kunyang’anywa mashamba yake, hatarejea CCM hata akinyang’anywa mashamba yote aliyoanayo.

Sumaye alihama CCM mwaka jana, miezi michache kabla ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu na kujiunga na harakati za kumpigia kampeni mgombea urais kwa tiketi ya Chadema, Edward Lowassa. Baada ya uchaguzi huo alitangaza kujiunga rasmi na Chadema.