Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU imempandisha mahakamani kigogo mmoja wa mamlaka ya elimu nchini TEA Bw. Isaya Paul kwa makosa 330 ambayo yameisababishia serikali hasara ya zaidi ya shilingi milioni 560.
Kigogo huyo ambaye amepandishwa katika mahakama ya hakimu mkazi Kinondoni mbele ya hakimu mfawidhi Frank Moshi amesomewa mashtaka hayo na wanasheria wawili kutoka TAKUKURU Bi .Faraja Samale na Bi. Vero Ndeoya ambao katika mashtaka hayo wameiambia mahakama kuwa katika nyakati na tarehe tofauti kwa mwaka 2011 na 2013 mshtakiwa huyo aliiba fedha za serikali kupitia benki ya CRDB tawi wa Kijitonyama wakaongeza kuwa mtuhumiwa huyo alifanya hivyo akijua wazi kuwa ni kosa kisheria na hasa kwa yeye ambaye ni mtumishi wa umma mwenye dhamana kubwa ya kutunza na kufanya matumizi sahihi ya fedha ambazo zilikuwa ndani ya dhamana yake yeye.
Aidha mahakama ikaambiwa kuwa mtuhumiwa huyo mbali na kufanya wizi kupitia benki hiyo ya CRDB pia kwa nyakati tofauti tofauti katika maeneo yasiyojulikana amekuwa akighusihi hundi mbalimbali za mamlaka ya elimu nchini na kujipatia fedha kwa kudai kuwa hundi hizo ni halali akiwa kama mfanyakazi wa mamlaka hiyo.
Mshitakiwa huyo amekana makosa yote 330 ambapo kupitia wakili anayemtetea Bw .Agustino Kusalikwa ameiomba mahakama kumpatia dhamna mteja wake huyo lakini hakimu Mh. Moshi akasema kwa mujibu wa sheria kwa kosa ambalo linahusisha fedha zaidi ya shilingi milioni kumi mahakama hiyo haina uwezo wa kutoa dhamana na hivyo mshtakiwa yupo ndani hadi novemba 14 mwaka huu.