Ili kupambana na wizi na ujambazi na aina mbalimbali za uhalifu, mkuu wa wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri amepiga marufuku kampuni za ulinzi kuwa na walinzi raia na
badala yake kutoa ajira kwa Migambo waliofuzu mafunzo ya
uaskari.
Mkuu wa wilaya ya Njombe, Ruth Msafiri (kushoto)
Msafiri ametoa kauli hiyo wakati akifunga mafunzo ya mgambo, katika kata ya Kifanya ambapo askari wa akiba zaidi ya 150 wamefuzu mafunzo ya uaskari kwa ajili ya ulinzi wa raia na mali zake.
Mhe. Msafiri amesema kuwa watafanya uhakiki wa kuhakikisha kampuni zote na maeneo yote yanayolindwa na walinzi wanakuwepo walinzi waliopitia mfunzo kwa usalama wa maeneo hayo lakini pia ni fursa ya ajira kwa wahitumu wa mafunzo hayo.
Katika risala yao wahitimu hao wa mafunzo ya mgambo wametoa ombi kwa mkuu wa wilaya hasa juu ya upatikanaji wa ajira na kuboreshewa mitaala ya mafunzo hayo.
Baada ya kumalizika kwa mafunzo hayo, wilaya ya Njombe itakuwa na askari wapya wa akiba zaidi ya 500 ambapo kwa kawaida kila mwaka ni askari 100 ndiyo wanaopata mafunzo hayo.