Mahakama Yaamuru Jide Awaombe Msamaa Viongozi wa Clouds 

Mahakama ya Wilaya Kinondoni leo Jumatano, Novemba 2, 2016, imemtia hatiani mwanamuziki nguli wa Bongo Fleva, Judith Wambura Mbibo “Lady Jaydee” (pichani juu) kwa kutoa maneno ya kashfa dhidi ya viongozi wa Clouds Media Group Joseph Kusaga na Ruge Mutahaba. Mahakama hiyo imemuamuru aombe radhi kupitia kwenye chombo cha habari chenye “coverage” kubwa nchini kote na ikiwezekana duniani.
Joseph Kusaga.
 Katika kesi hiyo, Jaydee anashtakiwa na viongozi wa Clouds Media Group ambao ni Mkurugenzi wa Kampuni hiyo Joseph Kusaga na Mkurugenzi wa Utafiti wa Redio hiyo, Ruge Mutahaba kwa kuuchafua uongozi wa kampuni hiyo na viongozi wake kupitia mitandao ya kijamii katika malumbano makali kati ya pande hizo mbili. 
Ruge Mutahaba.
Mei 2013, Clouds Media Group na Ruge walimburuza Jaydee mahakamani kwa kile walichodai kwamba alikuwa akiwatukana kwenye mitandao ya kijamii. Katika kesi inayomkabili msanii Judith Wambura Mbibo maarufu kama Lady Jay Dee dhidi ya walalamikaji Joseph Kusaga na Ruge Mutahaba kesi namba 29 ya Mwaka 2013 hukumu yake imetolewa leo na Hakimu wa mahakama ya Wilaya Boniphace Lihamwike kuwa wameridhishwa na ushahidi uliotolewa kuwa msanii huyo alitenda kosa la kuwadhalilisha na kuwakebehi kwa maneno machafu ndugu Joseph Kusaga pamoja na Ndugu Ruge Mutahaba.
 Hhivyo Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni imeamuamuru msanii huyo kuomba radhi katika chombo cha habari cha kitaifa au kinachosikika kimataifa pamoja na duniani nzima kuwa maneno yake yalikuwa ya kashfa na udhalilishaji yenye lengo la kuichafua taswira nzuri ya ndugu Kusaga pamoja na ndugu Ruge Mutahaba vilevile Mahakama imemuamuru Jide msanii huyo kulipa fidia na gharama za uendeshwaji wa kesi hiyo. Hukumu ya kesi hiyo iliyosomwa leo saa 2:30 asubuhi katika Mahakama ya Wilaya Kinondoni upande wa Msanii Judith Wambura uliwakilishwa na Wakili wake aitwaye Advocate Chacha licha ya msanii huyo kuhudhuria mahakamani hapo na kushindwa kushuka kwenye gari aina ya Noah waliyokuwa wamefika nayo Mahakamani hapo akiambatana na Meneja wake Seven Mosha ambaye alizuiliwa getini na walinzi kutokana na kuvaa nguo isiyozingatia maadili ya Mahakama.
 Mwenendo wa kesi hiyo iliyofunguliwa tangu mwaka 2013 kwa msanii huyo akituhumiwa kuwatukana, kuwakebehi pamoja na kuwakashifu ndugu Joseph Kusaga pamoja na Ruge Mutahaba kupitia mitandao ya kijamii na mahojiano aliyokuwa akifanya mara kwa mara na vyombo tofauti vya habari. Tangu kesi hiyo ilipofunguliwa msanii huyo amekuwa na mwenendo usiokuwa wa kuridhisha na kumfanya kushindwa kesi hiyo ni pamoja na; 1. Kukosa ushahidi wa yale aliyokuwa akiyazungumza yeye binafsi kwamba ametendewa na kufanyiwa na washtaki, 2. Kukosa mashahidi wa kusimama mahakamani kutetea alichokuwa anakisema kwani mpaka kesi inamalizika hakuweza kuleta shahidi hata mmoja. upande wa washitaki uliweza kuleta mashahidi takribani 15 mpaka hukumu ya kesi inasomwa hii Leo.
 3. Kutokuhudhuria mahakamani yeye mwenyewe, jambo linalotafsiriwa na wengi kama kutokuwa makini lakini pia kukurupuka kwa yale aliyokuwa akiyasema na kuandika kwani inawezekana kabisa sababu tajwa hapo juu zilimfanya aingie mitini. Moja kati ya maneno yaliyomtia hatiani Jaydee ni wosia aliouandika May 2013 kupitia blog yake. Wosia huo ulisomeka:
 Watu wanashtuka mtu akiongelea kifo, Utafikiri hawafahamu fika kuwa kila nafsi itakionja, Kwenye maisha yangu nimepitia mambo mengi, magumu na mepesi. Na bado naendelea ku experience mambo magumu zaidi kadri ninavyozidi kuwa mkubwa. Siku za karibuni nimekuwa nikipigwa vita sana na watu wenye uwezo mkubwa kifedha ,
 ki umri na hata wenye ukubwa wa connection katika hii industry ya muziki. Wanaomiliki chombo cha habari. Nasimama na kusema kuwa sitokata tamaa, kwani lengo lao kubwa ni kuona na kuhakikisha nimeanguka kabisa na sipo katika ramani ya muziki. Watu hao ambao vita yao ilikuwa baridi miaka kumi iliopita, sasa inazidi kuwa moto baada ya kutambua kuwa mimi ni mtu mwenye maamuzi yangu na misimamo yangu bila kuburuzwa. Wanapita kila mahali kuhakikisha kila mrija unaoniingizia chochote unakatika, na hiyo ni kutaka kuuthibitishia umma wa Tanzania kuwa hakuna msanii anaeweza ku survive bila wao
Mimi ni msanii tofauti na hao mnaofikiria. Nadhani mnafahamu tangu niachane na Tuzo zenu mnazo influence nani apate nani asipate, na tangu niachane na Fiesta nilipolipwa laki 8 mara ya mwisho na kuamua kuunda Band ili nijiajiri na kupata shows zangu mwenyewe, ikafanikiwa sana jambo ambalo limewauma na kuamua kufanya kitu cha kuiangusha Band yangu.

 Nita survive kwa njia zozote MUNGU alizonipangia. Wakati bado wote tunapumua na kwakuwa watu hao hawanipendi kabisa, Naamini fika hawataweza kunipenda hata siku nitakapokuwa nimekufa. Na huu ndio wosia wangu kwa watu hao. Natambua wanaweza kutumia redio yao kutangaza sana kifo changu na kusema marehemu alikuwa mtu mzuri na pengine kupiga nyimbo zangu kuanzia asubuhi mpaka jioni. Ila naomba nitamke hivi, siku nikifa CLOUDS FM isipige nyimbo zangu, wala isiongelee lolote kuhusiana na kifo changu. Ruge Mutahaba na Joseph Kusaga wasihudhurie msiba wangu, na mkiwaona muwapige. Enyi mtakaokuwa hai baada yangu. Kama wamenifitini, na hawajanipenda nikiwa hai. Hakuna haja ya kujifanya kunipenda nikiwa marehemu. Sina haja wanipende pia kwakuwa mimi sio ndugu yao, Ila ubaya wanaoundeleza mioyoni mwao wanaujua na nina hakika nafsi zao zinawasuta pia.
 Niliamua kujiepusha nao miaka mingi na kufanya biashara zangu, nimekaa kimya watu wanafikiri nabebwa lakini sijabebwa chochote sikutaka ugomvi haya mambo yalianza baada ya Album yangu ya pili ya Binti mwaka 2003 nilipojitoa Smooth Vibes chini ya Ruge. Nilivumilia fitna nikiamini ipo siku yatakwisha lakini naona moto ndio unazidi kuwaka. Na hii ni kwasababu wanaogopa msanii akiwa mkubwa watashindwa kumuamrisha, Hamuwezi kumiliki dunia.. Kama mnasema mlinibeba mbona hamkuwabeba dada zenu wa tumbo moja waimbe ili hela irudi nyumbani??. kama kweli wewe Kusaga unajua kubeba basi beba jiwe liimbe liwe star..

 Kwa roho zenu mbaya mnaweza kumbeba mpita njia nyie??. Talent haibebwi, hujibeba kama mnabisha si mna watoto wabebeni basi wawe kama kina Diamond ndio nitaamini kweli nyie mnaweza kubeba watu. Mnawatishia wasanii kuwa yoyote atakaefanya nyimbo na mimi hazitapigwa, vikao vinne mmeshakaa kunijadili. Mnadhani je! nitapungukiwa nini endapo wasanii wengine wakiacha kufanya kazi na mimi??
 nyimbo hazitakuwa nzuri. Basi sawa ngoja tuone MUNGU ni nani, Binadamu nani?? Kwahiyo mtaamrisha watu pia wasikae na mimi?? Ilikuwa niseme majina matatu huyo mmoja nimemsamehe baada ya kugundua sio hiyari yake ila yuko under influence ya hawa jamaa wawili. Kila siku mnamsingizia Ruge peke yake Kusaga ni mfitini kuliko hata huyo Ruge, watu hamjui tu. Mtu hela zote hizo bado shillingi mbili ya Jide inakuuma?? Roho gani hiyo?? Naishia hapo na sitabatilisha kauli yangu. Licha ya hukumu hiyo kutolewa, Meneja wake, Seven Mosha, amesema kuwa Lady Jaydee atatoa maelezo yake kuhusu hukumu hiyo muda si mrefu