SERIKALI YATAJA MAREKEBISHO SABA KATIKA MUSWADA WA SHERIA YA HUDUMA ZA HABARI 2016

Serikali jana imewasilisha bungeni muswada wa sheria ya huduma za habari mwaka 2016, huku ikitaja marekebisho saba katika muswada huo. 

Marekebisho hayo ni pamoja na kuainisha haki na wajibu wa wanahabari, kuainisha haki ya chombo cha habari kukata rufaa, uwakilishi wa wanahabari katika bodi ya ithibati, Jaji Mkuu kuweka utaratibu wa kusikilizwa haraka kesi za kashfa. 

Mengine ni kuviondolea vyombo vya habari adhabu kwa baadhi ya makosa ya mwandishi, vyombo vya dola kukamata mitambo na vifaa vya wanahabari na mitambo kutohusika moja kwa moja kwa kosa la gazeti. 

Akiwasilisha bungeni muswada huo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, alisema marekebisho hayo yamefanyika baada ya mashauriano na wadau wa habari wakiwamo wananchi, wanataaluma ya habari, wanasheria na kamati nyingine za bunge. 

Alisema katika eneo la kuainisha haki na wajibu wa wanahabari, muswada wa awali kwa kiasi kikubwa uliainisha zaidi wajibu wa wanahabari lakini kwa kuzingatia mikataba ya kimataifa ambayo nchi imesaini na kuridhia na matakwa ya katiba. 

Nnauye alisema kwa sasa eneo hilo limerekebishwa katika kifungu cha saba kwa kuainisha pia haki za wanahabari kama vile uhuru wa kukusanya, kuhariri na kuchapisha au kutangaza habari. 

Alisema kuhusu kuainisha haki ya chombo cha habari katika kukata rufaa, katika kifungu cha 10 kuhusu utoaji wa leseni za vyombo vya habari , muswada wa awali haukuwa umeweka haki ya kukata rufaa kwa atakayekataliwa kupewa leseni na Mkurugenzi wa Idara ya Habari. 

Alibainisha kuwa chombo husika kinaweza kukata rufaa kwa waziri wa habari na pia mwishowe kisiporidhika na uamuzi wa waziri sasa kinaweza kupinga suala hilo mahakamani. 

Kuhusu uwakilishi wa wanahabari katika bodi ya ithibati, Nnauye amesema eneo hilo limeboreshwa ni uwakilishi wa vyombo vya habari katika bodi hiyo, na kwa mujibu wa mapendekezo ya awali, bodi hiyo itakayokuwa na wajumbe saba sasa itakuwa na wanahabari wanne akiwemo mwenyekiti. 

Alisema suala la Jaji Mkuu kuweka utaratibu kusikilizwa haraka kesi za kashfa, moja ya malalamiko makubwa ya wadau katika utoaji wa haki zinapokuja kesi za habari hasa za masuala hayo ni kuchukua muda mrefu kwa kesi hizo. 

Katika maboresho ya kipengele hicho, alisema hivi sasa jaji huyo kwa kuzingatia tathmini ya uwezo wa Mahakama na rasilimali zilizopo na kama ilivyowekwa kwa kesi nyingine kama za uchaguzi atatunga kanuni zitakazoweka muda wa kumalizika kwa kesi za aina hiyo. 

Kadhalika, Nnauye alisema kuhusu vyombo vya dola kukamata mitambo na vifaa vya wanahabari, maboresho yamefanywa kwa kulenga kumuondoa mkurugenzi wa idara ya habari kuwa na mamlaka ya kukamata mitambo hiyo.