MAKACHERO wanaochunguza mauaji ya kikatili ya aliyekuwa mwalimu mkuu wa Shule ya Upili ya Kiru nchini Kenya Bw Solomon Mwangi sasa wanamwandama afisa wa upelelezi wa Jinai anayehudumu katika Kaunti ya Nairobi.
Wameambia Swahilihub kuwa kachero huyo anayefanya kazi katika kituo cha polisi cha Kasarani huenda 'ana habari muhimu za kutuwezesha
kutegua kitendawili cha mauaji hayo'.
Pia makachero hao wanamwandama mwanamke ambaye huhudumu katika duka la huduma ya kuweka na kutuma pela ya M-Pesa mjini Kiriaini.
Mwanamke huyo anadadisiwa kwa lengo la kupata habari muhimu kuhusu mauaji hayo.
Bw Mwangi alipatikana akiwa ameuawa kikatili katika shamba la kahawa la Karuntuma lililoko karibu na mtaa wa Witeithie katika barabara kuu ya Nairobi kwenda Thika.
Mwili wake ulikuwa na majeraha mabaya.
Alikuwa ameng'olewa meno na jicho la kushoto lilikuwa limetolewa. Alikuwa amegongwa usoni mara kadhaa kwa kifaa butu kabla ya kuuawa kupitia kunyongwa.
Alitoweka Novemba 5, siku ya kuanza kwa mtihani wa KCSE na maiti yake ikapatikana Novemba 11.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa upelelzi wa Jinai katika Kaunti ya Murang’a Bw Stephen Chacha, wawili hao wametajwa kwenye awamu ya kwanza ya uchunguzi.
“Awamu hii haimaanishi kwamba tayari wana habari za kuwahusisha na mauaji hayo. Uchunguzi huchukulia kila aina ya habari kwa uzito na ni lazima anayetajwa aweze kuchunguzwa,” akasema.
Mpenzi wa mke wa marehemu
Amesema kuwa kachero huyo wa Kasarani ametajwa kuwa mmoja wa wapenzi wa mke wa marehemu, Bi Jane Mwangi.
Tayari, Bi Mwangi anazuiliwa na maafisa wa polisi hadi Novemba 21 baada ya kushtakiwa mahakamani Murang’a kama mshirika mmoja wa mauaji hayo ya mumewe.
Bi Mwangi anadaiwa kuwa alikodisha gari alilombeba nalo marehemu hadi eneo la mauaji. Gari hilo pia limenaswa na makachero na linachuziwa katika makao makuu ya polisi Murang’a.
Bw Chacha aliambia Swahilihub kuwa “kuna madai kuwa Bi Mwangi ambaye alikuwa mwalimu mkuu wa Shule ya Upili ya Ichachiri katika kaunti ndogo ya Gatundu alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na kachero huyo.”
Kwa upande mwingine, marehemu naye alidaiwa kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mhudumu huyo wa Mpesa, hali ambayo inawafanya makachero hao kuchunguza iwapo mtandao huo wa kimapenzi unaweza kuwa na
ushawishi wowote katika njama ya kumwangamiza Bw Mwangi.