TANZIA: MTOTO ALIYEFANYIWA UPASUAJI WA KUPANDIKIZA BETRI MOYONI AFARIKI DUNIA


Mtoto Happiness Josephat (6) aliyefanyiwa upasuaji wa kupandikiza betri moyoni katika Taasisi ya Tiba ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI), amefariki dunia. Alithibitisha mama mzazi wa Happiness, Elitruda Malley kwa njia ya simu na kusema kwamba Happiness alifariki dunia ghafla juzi mchana.

Mama Happiness alisema Jumapili, mtoto huyo alikuwa mzima na walikwenda kanisani kutoa sadaka ya shukrani kama ishara ya kumshukuru Mungu kwa mambo aliyowatendea na wakarudi nyumbani salama na ghafla hali yake ilibadilika akaanza kulalamika kuwa anajisikia vibaya, na kukimbizwa Hospitali ya Selian mjini Arusha na wakiwa njiani alifariki dunia.

Happiness alikuwa tayari amesharudi shuleni, na alisema atasoma kwa bidii ili kutimiza ndoto yake ya kuwa daktari bingwa itimie aweze kusaidia watu wanaosumbuliwa na magonjwa mbalimbali.

maziko ya Happiness yanatarajiwa kufanyika leo huko Mbulu mkoani Manyara.



Happiness alifanyiwa upasuaji huo wa historia nchini Julai 15, mwaka huu katika Taasisi ya JKCI wa kuwekewa betri maalumu kwenye moyo ambayo kitaalamu inaitwa ‘pacemaker’.

Kwa mujibu wa madaktari waliokuwa wakimtibia mtoto huyo, wakati alipopekekwa hospitalini hapo, mapigo yake ya moyo yalikuwa 20. Pia walisema hali hiyo kwa mtoto si ya kawaida kwa vile anapaswa kuwa na wastani wa mapigo 60 hadi 100 kwa umri wake. Mtoto Happiness alizaliwa na tatizo hilo ambalo mara nyingi hali hiyo huwakumba watu wazima.