Siku kadhaa baada ya utabiri wa TB Joshua kuwa Hillary Clinton angeshinda urais wa Marekani kuwa tofauti, hatimaye mhubiri huyo maarufu wa Nigeria ametoa ufafanuzi kuhusu kilichotokea.
Awali, TB Joshua aliwaambia waumini wake kuwa aliona ndotoni kuwa Rais wa Marekani atakayechaguliwa atakuwa mwanamke na kwamba atakumbwa na changamoto nyingi ikiwemo jaribio la kutaka kumuondoa madarakani kwa kura za kutokuwa na imani naye.
Mhubiri huyo ametumia ukurasa wake wa Facebook na Twitter kuutetea utabiri wake akidai kuwa Clinton alishinda kupitia kura za jumla, kwa kupata kura nyingi zaidi ya Donald Trump.
“Tumeona matokeo ya uchaguzi wa Marekani. Kwa kusoma, utagundua kuwa [utabiri]ule ulikuwa kuhusu kura za jumla (popular votes), kura za wamarekani wengi,” unasomeka ujumbe wa TB Joshua.
“Katika hali hii, tunahitaji roho ya kinabii kutambua au kujua unabii. Viwango vyetu ni tofauti. Hatuko kwenye viwango sawa. Tunaweza kuwa na makanisa makubwa, kengele kubwa, na shughuli zote ambazo ni nzuri kwa viwango vya kibidamu lakini uwezo wa binadamu una kikomo,” aliongeza.
Alitumia pia Biblia Takatifu kuupa nguvu utetezi wake, akitaja maandiko ya 1 Wakorinto 1: 25, “Maana kinachoonekana kuwa ni upumbavu wa Mungu, kina busara zaidi kuliko hekima ya binadamu; na kinachoonekana kuwa ni udhaifu wa Mungu, kina nguvu zaidi kuliko nguvu za binadamu.”
Clinton alishinda kwa kupata kura nyingi zaidi za Wamarekani (popular votes) lakini alishindwa katika kura za majimbo muhimu (electoral votes). Mgombea wa Republican ambaye tafiti nyingi hazikumpa nafasi, alishinda uchaguzi huo na kuishangaza dunia.
Trump anatarajiwa kuapishwa rasmi kuwa Rais wa Marekani, Januari mwakani.