Upinzani wahoji serikali kwa mpigo

KAMBI rasmi ya upinzani ya Bungeni, imelalamika utaratibu unaofanywa na serikali wa kupeleka marekebisho mengi kwa mpigo, na ya sheria nyingi katika muswada mmoja licha ya kuonya athari zake wakati wa bunge lililopita.

 Msemaji wa kambi hiyo katika Wizara ya Katiba na Sheria, Tundu Lissu, akiwasilisha maoni ya kambi rasmi ya upinzani kuhusu Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa 2016, alisema kambi hiyo imekuwa ikilalamika mara kwa mara kuhusu uwasilishaji wa marekebisho mengi kwa wakati mmoja.

 “Utaratibu huu, unalinyima Bunge muda na uwezo wa kuyajadili kwa kina na kuyaelewa mapendekezo ya serikali kabla ya kuyapitisha na kuwa sheria ya nchi,” alisema Lissu. Lissu alisema matokeo ya utaratibu huo si tu ya kuligeuza Bunge kama muhuri au chombo cha kupitisha kila jambo na kuhalalisha uamuzi wa serikali, bali pia yanasababisha Bunge kupitisha sheria mbovu zinazoathiri haki za wananchi na ustawi wa taifa. 

Pia alisema hali hiyo husababisha migongano isiyo ya lazima 
katika vyombo vya utekelezaji vya umma. Alisema katika maoni ya kambi hiyo kwenye bunge lililopita, waliishauri serikali kuacha utaratibu huo wa utungaji sheria kwa kuwa utachangia kuzalisha sheria mbovu za nchi. 
Msemaji huyo alisema kutokana na utaratibu huo, kambi ya upinzani inamwomba Spika atumie mamlaka yake kuhakikisha utaratibu bora zaidi wa utungaji sheria unafuatwa. 
Alisema utaratibu bora unaotakiwa ni ule unaliolipatia Bunge muda wa kutosha wa kujadili Miswada ya Sheria kabla ya kuipitisha na kuwa sheria, huku mapendekezo ya marekebisho makubwa ya sheria yoyote yakitakiwa kuwasilishwa kwa njia ya muswada wa marekebishio ya sheria husika badala ya kuyaficha.

 MARA YA PILI Lissu alisema hiyo ni mara ya pili kwa Sheria ya Mikopo, Misaada na Dhamana za Serikali kufanyiwa marekebisho makubwa, mara ya kwanza ikiwa Aprili 3, 2003 wakati Bunge hilo likipitisha sheria ya marekebisho ya sheria hiyo. 
“Sheria hiyo iliongeza vifungu vipya 12 katika sheria mama iliyokuwa na vifungu 23 awali,” Lissu alisema kupitia kauli hiyo ya kambi rasmi ya upinzani Bungeni. Hata hivyo, alisema muswada huo unapendekeza marekebisho makubwa zaidi ya sheria hiyo, ikiwa na vifungu 21 kati ya 35 vya sheria vinapendekezwa kurekebishwa.

marekebisho ya sheria mbalimbali. Aidha, alisema kifungu cha tatu cha sheria mama kinampa waziri mwenye dhamana ya masuala ya fedha, mamlaka ya kuingia mikataba ya kupata mikopo kutoka nje kwa niaba ya serikali kwa masharti ya riba, utaratibu wa malipo au itakavyokubaliwa. Lissu alisema kambi rasmi ya upinzani bungeni,
 inafahamu katika mazingira ya matumizi ya maneno ‘mkopo wowote unaokopwa na serikali kutoka vyanzo visivyokuwa vya ndani’ yana maana mikopo yote inayopatikana kutoka serikalini, benki na taasisi zingine za kifedha zilizo nje ya nchi. 

“Hii ina maana mkopo huo unaokopwa na serikali kutoka vyanzo vya ndani ni kuwa ni ile inayopatikana kwa mabenki ya kibiashara na taasisi nyingine za fedha zilizopo ndani ya nchi,” alisema. Hata hivyo, alisema kambi hiyo inaunga mkono maoni na ushauri uliowasilishwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria kuhusu muswada wa sheria ya marekebisho ya sheria mbalimbali (Na. 4) wa 2016.