Samsung imelazimika kusitisha utengenezaji wa simu za Galaxy Note 7 kutokana na tatizo lake la kulipuka.
Kampuni hiyo ya Korea Kusini, Jumanne hii iliamua kusitisha kimoja utengenezaji wa simu hizo, saa chache baada ya kuwaambia wateja wasitumie tena simu hizo.
Kufuatia tangazo hilo, hisa zake zilishuka kwa asilimia 8, na kupunguza dola milioni 17 za thamani yake sokoni.
Simu hiyo ilipangwa kuwa mshindani wa iPhone 7, lakini badala yake imekuja kuharibu vikali heshima ya Samsung. Wachambuzi wanadai kuwa uamuzi wa Samsung kuipiga chini Note 7 moja kwa moja – itasababisha hasara ya dola bilioni 9.5 za mauzo na kupoteza faida ya dola bilioni 5 za faida.
Kwenye maelezo yake ya mwanzo, Samsung ilisema itayaomba makampuni na mawakala wake dunini kote kuacha mauzo ya Galaxy Note 7, wakati inachunguza chanzo cha kushika moto. Iliwaomba pia wateja wenye simu za awali za Galaxy Note 7 au zile walizobadilishiwa, kuzizima na kuacha kuzitumia kabisa.
Hatua hiyo imekuwa na matokeo hasi kibiashara kwa kampuni hiyo ya Korea Kusini. Mapema September, Samsung ilizirudisha kiwandani simu milioni 2.5 kutoka duniani kote na kuanza kutoa simu mpya kufidia, ambazo nazo zimegundulika kuwa na tatizo la kushika moto.
Jumatano iliyopita, moshi ulianza kutoka kwenye Galaxy Note 7 mpya kwenye ndege ya Southwest Airline kabla haijapaa na kulazimika kusitishwa kwa safari.