Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Nape Moses Nnauye ameipongeza klabu ya Simba kwa kuomba radhi kufuatia mashabiki wake kuvunja viti zaidi ya 1700 katika uwanja wa Taifa na kuahidi kuvitengeneza.
Akiongea katika kipindi cha 5Sports cha EATV, Nape ameonyesha kusikitishwa kwake juu ya utovu wa nidhamu uliooneshwa na mashabiki wa soka jambo ambalo limesababisha serikali kufungia timu za Simba na Yanga kucheza katika uwanja huo wa Taifa.
“Naipongeza Simba kwa kuomba radhi kutokana na kitendo kilichofanywa na mashabiki wake na kwa sasa timu hizo zitacheza katika uwanja wa Uhuru, ili kutoa funzo kwa watumiaji kutambua thamani ya uwanja na kuheshimu mali za umma, serikali imelazimika kuchukua maamuzi hayo ili kuondokana na adhabu za kimazoea, na pia tuna mpango wa kufunga kamera uwanjani ili kubaini wahusika moja kwa moja badala ya kuishia kuziadhibu timu” Amesema Nape.
Pamoja na hayo Waziri Nape amesema serikali haikutaka kuunda kamati ya uchunguzi katika sakata hilo kwa madai kuwa kuunda kamati ni kupoteza pesa, raslimali na muda hasa kwa jambo ambalo lilionekana hadharani machoni pa watu wengi.
Aidha Waziri amesema asilimia 98 ya uwanja wa Uhuru umejengwa kwa saruji katika maeneo ya kukalia, hivyo mechi za Simba na Yanga ni ruksa kufanyika katika uwanja huo.
Baada ya tukio la mashabiki wa Simba kuvunja viti uwanjani, Msemaji wa Simba Haji Manara alijitokeza hadharani na kuomba radhi kwa watanzania kutokana na kadhia iliyosababishwa na mashabiki baada kutoridhia maamuzi ya mwamuzi Martin Saanya kuhusu goli lililofungwa na Amisi Tambwe.